
Na Abbas Mwalimu (0719258484).
Alhamisi , 4 Novemba, 2021.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametimiza mwaka mmoja tangu alipoapishwa kushika madaraka ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi tarehe 2 Novemba, 2020.
Katika kipindi cha mwaka mmoja licha ya dunia kukumbwa na janga la UVIKO 19 lakini kuna jambo moja kubwa kati ya mengi ambayo Mheshimiwa Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi amefanya akiongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kama ilivyobainishwa kweye ibara ya 9 ibara ndogo ya 3 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 toleo la 2010.
Kwa mtazamo wangu jambo hili ndilo muhimu zaidi kwani ndilo linalobeba mhimili wa mafanikio na sura mpya ya Zanzibar.
Ni suala gani hili?
Jambo hili ni Kujenga Kuaminiana (Trust Building)
Historia ya Zanzibar tangu uchaguzi wa mwaka 1995 mpaka 2015 inaonesha kuwa kumekuwa na hali ya kutoaminiana baina ya vyama vyenye nguvu za ushawishi katika siasa za visiwani jambo lililopelekea kuzuka kwa vurugu katika chaguzi, kusuasua kwa serikali ya umoja wa kitaifa (SUK) na hata kusababisha vifo na ulemavu kwa watu kutokana na vurugu zinazojitokeza baada ya matokeo ya uchaguzi (Cheeseman 2011; Mehler, 2009; Minde, 2018)
Kutokana na historia hiyo suala la kujenga kuaminiana linaonekana kuwa na umuhimu wa kipekee katika kuwaunganisha Wazanzibari, kuleta amani, utulivu, mshikamano, umoja wa kitaifa na kuvutia uwekezaji.
Ni ukweli ulio wazi Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi amefanikiwa sana kuwaunganisha Wazanzibari, Wazanzibari hivi sasa wamekuwa kitu kimoja kwa asilimia kubwa ukilinganisha na miaka kadhaa iliyopita. Hivi sasa watu wa itikadi tofauti wanakutana na kuzungumza, wanaswali pamoja, wanazikana na hata kutembeleana.
Hivyo katika kipindi cha mwaka huu mmoja Rais Mwinyi amefanikiwa katika hili la kujenga kuaminiana. Na katika kuhanikiza umuhimu wa kuaminiana Kelman (2005) alibainisha kwa kusema;
“Parties cannot enter into a peace process without some degree of mutual trust, but they cannot build trust without entering into a peace process.”
Kwamba, ‘Pande haziwezi kuingia kwenye mchakato wa amani ikiwa hakuna kiwango fulani cha kuaminiana, lakini pande hizo haziwezi kujenga kuaminiana pasina kuingia kwenye mchakato wa amani.’ Mwisho wa kunukuu.
Kwa kifupi ni kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya kuaminiana, amani na maendeleo. Kwa mantiki hiyo utekekezaji wenye ufanisi wa Sera ya Uchumi wa Buluu unategemea sana uwepo wa mambo haya matatu sambamba na utulivu, umoja na mshikamano wa Wazanzibari ambao unaonekana hivi sasa ambao unatokana na uwepo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Lakini ni kwa kiasi gani wananchi wanafahamu Serikali ya Umoja wa Kitaifa? Hili ni swali ambalo watendaji na wasaidizi wa Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi wanapaswa kujiuliza.
Kwa wengi serikali ya Umoja wa Kitaifa inatafsirika kama Serikali ya Makubaliano baina ya vyama viwili vikubwa visiwani, jambo ambalo nadhani linaleta changamoto ya ufahamu.
Lakini wengine wanaamini kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni baina ya viongozi watatu yaani Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Makamu wake wa Kwanza Mheshimiwa Masoud Othman Masoud Sharif na Makamu wake wa Pili Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla. Tafsiri hii pia inafanya wananchi wasifahanu nafasi yao katika serikali.
Kutokufahamu tafsiri sahihi kunaifanya jamii kutofahamu haki na wajibu wao katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Kwa mujibu wa Mukoma (2008), wananchi wana haki na wajibu wa kuishauri, kuikosoa (kwa heshima) serikali yao na pia kushiriki katika maendeleo ya pamoja. Hivyo serikali ya umoja wa kitaifa ni ya kila mwananchi na si kundi fulani au pande fulani pekee kama baadhi ya watu wanavyodhani.
Ushiriki wa wananchi na ushirikiano baina yao na ushirikishwaji katika ujenzi wa taifa unaondoa uwezekano wa kutokea kwa migogoro na mgawanyiko baina ya wananchi hasa kutokana na kuhusisha jamii zote katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.
Mukoma (2008) ameendelea kubainisha kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ina wajibu wa kupeleka maendeleo sawa kwa watu wote na kugawanya sawa keki ya taifa.
Nafahamu mwaka mmoja ni mdogo kupima mafanikio lakini katika hili la kujenga kuaminiana (Trust Building) baina ya Wazanzibari, Mheshimiwa Dkt. Mwinyi amefanikiwa sana ingawa bado ana kazi kubwa ya kuongeza kuaminiwa kwake kwa kuhakikisha kunakuwa na usawa na haki zaidi kwa Wazanzibari wote, wananchi wanapata huduma za msingi kama afya (bima ya afya kwa wote), barabara, maji, umeme, elimu bora sambamba na kuondoa changamoto mbalimbali zilizobainishwa katika vipindi vilivyopita.
Hivyo basi, kwa maoni yangu ni kwamba Mheshimiwa Dkt. Mwinyi amefanikiwa sana kuleta hali ya kuaminiana (Trust) kitu ambacho ni muhimu sana katika ujenzi wa Zanzibar mpya lakini pia nadhani kuna haja ya kuhakikisha wananchi wanafahamu tafsiri pana ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuanzia ngazi ya Masheha, Umuhimu wake na hata mambo yanayoweza kupelekea kuvunjika kwake ili wananchi wabebe jukumu la kulinda mafanikio yaliyopatikana.

Albert Einstein alipata kusema na ninamnukuu, “There is no peace without trust” kwa tafsiri yangu isiyo rasmi, ‘Hakuna amani pasina kuaminiana.’ Hivyo hili la kujenga kuaminiana alilolijenga Rais Mwinyi ni kubwa mno na ndiyo nguzo kuu ya maendeleo ya Zanzibar wakati huu Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Hussein Mwinyi ikitekeleza Sera ya Uchumi wa Buluu Zanzibar.
Wenu:
Abbas Mwalimu
(Facebook|Instagram|Twitter|Clubhouse).
+255 719 258 484
Uwanja wa Diplomasia
(Facebook|WhatsApp).